UGANI ni jukwaa la ubunifu wa kidijitali lililosheheni hazina ya maarifa yaliyotafitiwa ya kilimo na sayansi zinazohusiana na kilimo. Ni mtandao wa kijamii unaotoa huduma za usambazaji wa taarifa kwa ushiriki ili kuboresha maisha ya jamii za vijijini nchini Tanzania na kwingineko. Tovuti hii pia inaonesha video za mafunzo ya kilimo kwa Lugha ya Kiswahili na inatoa mafunzo kwa njia ya mtandao kwa wakulima ili kuwasiliana na Maafisa Ugani. Hili ni jukwaa la wafanyakazi wa Utafiti na Uendelezaji kilimo, watoa huduma, wakala wa ugani, wasaidizi wa maafisa ugani, wahudumu wa mifugo, wataalam wa mawasiliano na wawakilishi wa mashirika ya wakulima.
Mradi umeanzishwa, unaendelezwa na kusimamiwa na shirika lisilolenga kutafuta faida liitwalo ‘The GardenFarm Institute’. Taasisi hii inabuni, inapanga na kuongeza thamani ya taarifa nyingi zilizopo katika kilimo na sayansi ya viumbe hai ili kuzifanya zipatikane, zitumike na zilete manufaa na tija.
Katika ‘The GardenFarm Institute’ tunaamini kwamba, taarifa za kidijitali zinaweza kuleta mageuzi katika namna ambavyo hivi sasa utafiti, elimu na ubunifu unavyosambazwa na kutawanywa katika jamii kwa kiasi kidogo. Pia tunaamini kuwa, mtandao ni kiwezeshi kikubwa cha kusaidia kubeba mageuzi haya na kwamba taarifa nyingi za kidijitali zinazopatikana katika mitandao hazijatumika vilivyo katika kuimua kilimo. Tunalenga mbali zaidi, katika kutatua matatizo halisi.
“Kwa sababu ya umuhimu wa Kilimo katika maendeleo yetu ingetegemewa kuwa Kilimo na mahitaji ya Wakulima yangekuwa ndio chanzo na kupewa kipaumbele katika utayarishaji wa mipango yote ya Uchumi wetu.Badala yake tumechukulia Kilimo kama sekta ya pembezoni au kama shughuli nyingine yoyote ya kawaida ambayo inatumiwa na sekta nyingine bila yenyewe kupewa umuhimu wowote ule…..Ni lazima sasa tuache kukipuuza Kilimo.Ni lazima tukifanye Kilimo ndio shina na mwanzo wa mipango yetu yote ya maendeleo.Kwani kwa hakika,Kilimo ndio msingi wa maendeleo yetu”
"Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K.Nyerere-1982"